
Ua hunyauka halafu Hujanyauka halafu, licha ya wake uturi Hakuko kuliko sefu, kote kunayo hatari Jua kali ukihofu, masika yana athari Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Kidhani shida ni mwamba, jaribu na kwenye mboji Karibu yote mashamba, mavuno bado hayaji K'athirika kama pamba, kifundiro sitaraji Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Mbegu lipandwa vema, tumaini ikazua Ardhini mewa hima, na mche ikaibua Meendeleza uzima, na kisha ikawa ua Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Ninalienzi waridi, lilivyo kweli nyerezi Linao umaridadi, na mng'ao kama mwezi Kuvutia inabidi, na kandoye kubarizi Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Wadudu wachavushaji, chavua huifikisha Wangepatiwa hojaji, ngewapa kukamilisha Kuhusu ujuaji, unaowafanikisha Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Matokeo ya chavua, ni umbo kulibadili Ua hilo kichanua, linaukosa utuli Wadudu wengi hutua, kufurahia asali Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Waridi lione kisha, taratibu lachuchuka Na chavua walokesha, waridi wamelichoka Sasa walidhalilisha, maninga yamefungika Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Ishiirini na saba, naenda zangu usono Mwezi ni wa oktoba, soma ushairi huno Ujumbe weka akiba, uthamini kila neno Hujanyauka halafu, hata ua lilo zuri Malenga wa Vilimani [email protected]) Oktoba 27, 2016

