
Kipya uzuri wake Magari mapya tayari, yamewasili mjini Madereva wenye ari, wakagua usukani Punde yawa ni vipuri, yale yetu ya zamani Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Yalosalia machache, mapya yawe yatawala Mara twasikia cheche, kwamba sijaze hawala Ati mapya ni mikweche, inayofaa kulala Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Yazoea tambarare, kuenda bila kusita Miteremko yanasare, na milima kutopita Waloyafanya yang’are, breki walizikataa Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Na ajikokote kobe, mwisho afike salama Kuliko mtu aibe, aogopwe kama duma Chuoni njia izibe, na moto wake kuzima Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Japo yana kila baya, uamilifu ni tele Si stani kungojeya, yakapakiwa mchele Talanta ufundi piya, bila shaka yako mbele Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Huo ndio umilisi, uwao kwa utendaji Ndiyo nguzo silabasi, uwezo ari vipaji Madereva tia kasi, wafikishe kwenye taji Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Ya zamani yamechina, yakakosa ushindani Hayapo kwa kila kona, yanalenga ofisini Tairi zao za dhana, hadhi yao si ya chini Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Kipya kweli kina nyemi, tena tiba ya kidonda Tungekuwa hatuhami, kama kweli tunatunda Kwayo mapya twajihami, panovuja kupaunda Kipya zuri upya wake, tupekue tuuone Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka)

