
Buriani Mtoto wa Mwalimu Sio tena siku njema, kidagaa kimeoza Siyo sauti ya mama, taanzia yatuliza Mauko yametufuma, Walibora kun'poteza Kuvunjika kwa mdomo, mate yanatawanyika Mtoto wa mualimu, metutoka Walibora Mbiu kaja kama bomu, kwamba kifo metupora Kusadiki ni vigumu, kuitikia kudura Tumebaki tuna pengo, kisa kung'olewa jino Kifo na mingi milango, kwa ajali metupoka Meathirika vitengo, fasihi na kadhalika Uli uti wa mgongo, ghafula umeondoka Haina kinga ajali, apendalo makuduri Kamanda wa Kiswahili, wa kikweli mzalendo Kiswahili kukidhili, ulipinga kwa vitendo Kandika kazi aali, zenye na mwingi uhondo Amri yake Rahimu, kattu haina rufani Titi mame kukomboa, liliona la kikati Kauli mbiu za doa, za kigeni ndizo ati Ajinabi kuvutia, kakataza si shuruti Kwani kila msafiri, huusifu mzigowe Itakuwa siku njema, kilazwa pema peponi Uupokee uzima, kwa rehema za Dayani Sauti tazidi vuma, kwa kazizo duniani Innalillahi! Najua, sote hapa twaondoka (Kelvin Kombo Motuka Malenga wa Vilimani) Nyamataro. Aprili kumi na sita, twenti twenti

