Song Cover Image

World Teachers Day - Heko! by Kelvin

Ni siku yenu walimu Walimu ni siku yenu, chachawa nyote walimu, Mwalimu kweli ni tunu, kazi yenu inadumu, Mwalimu sio fununu, mna mwingi ukarimu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe Walimu wangu mlipo, yangu someni nudhumu, Nitakuwa kama popo, kupingawo umuhimu, Taaluma tele zipo, yake mwalimu adhimu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe Mwalimu ndiye asili, nyingine zatoka humu, Mfinyanzi ndiye kweli, kubwa analo jukumu, Ajifunga silisili, bure anemshutumu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe Mwalimu daima nyota, mwanga kila sehemu, Aangaza kumemeta, wanafunzi azuumu, Ajinyima wakapita, halafu waje jikimu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe Hafikirii ujira, vyovyote kimdhulumu, Akose mafuta bora, maji atatayamamu, Mwalimu mwingi subira, hata walo chakaramu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe Una haki kufahiri, piga kifua mwalimu, Mchango wako dhahiri, japo watakuhukumu, Hana sababu nakiri, hasidi hino fahamu, Ni siku yenu walimu, kazi yenu ikumbukwe KELVIN KOMBO MOTUKA (Malenga wa Vilimani) Oktoba 5, 2021