Ase utu si mtu Utu ndilo jambo jema, ase utu mtu butu Uhayawani kivuma, utasemwa una kutu Kama lako ni kufuma, wakome wana wa watu Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Yateme mate ya fisi, ujiepushe papara Usiwe mtu bilisi, wa kupunja na kupora Rahisi haihalisi, watoto sio mpira Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Udhalimu kwa watoto, kote kote umechacha Limekuwa kama moto, kuenea kwa makucha Kuushinda sio ndoto, kama zake Alinacha Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Shuleni pawe pa heri, sigeuke jehanamu Wanafunzi wape ari, mshawasha wa elimu Udhalimu ni shubiri, juhudi zao husumu Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Haifai umwadhibu, kwa thabiti msimamo Mwalimu awe adibu, uigwe wake mfumo Sipalilie aibu, kutoza kwenye kisomo Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Kichapo hicho cha mubwa, si koporo unasema? Ni udhalimu mkubwa, na lazima utakoma Siogofye kama jibwa, hujaumbiwa dhuluma Mtu kuitwa ni utu, asiye utu si mtu Kelvin Kombo Motuka (Malenga wa Vilimani) KMF Twenty Nineteen