Likizo ya Madhehebu Kutoka nili mkembe, elewaye mazingira Nili nachezea nyembe, kaniachia madhara Kaparamia miembe, na mengi kutia fora Sijaona madhehebu, yamefungwa kwa likizo. Twaziona zote shule, vyuo na vyuo vikuu Zalikizwa tangu kale, kupumua angalau Kisa wanafunzi wale, matokeo yende juu Madhehebu yapo wazi, matokeo yakidoda! Mengi wala waumini, bila muda kumeng'enya Na chochote waamini, hata vile vya kusinya Wameshindwa kubaini, waona wote waponya Yanahitaji likizo, mafundisho kubukua. Lilokuwa utumishi, limekuwa ni kuchuma Tozo katu haziishi, wachochole kuwakama Hadhi ya juu waishi, madhabahu kisimama Badala ya kuangaza, jamii giza totoro! Muda wa kutafakari, waumini hawanao Waenda kama safari, wajae maabadio Katwani hawafikiri, yale ya ‘nabii' wao Wamesahau ukweli, wapewe likizo jama! Marudio yalazimu, tukumbuke akisami Mambo yaliyo muhimu, ya kiroho tujihami Sarakasi zisidumu, madhabahu kiuchumi Sasa twataka likizo, tulolila lielee. Likizoni Biblia, asome mkiristu Mwenyewe kuibukua, asibaki kuwa butu Kurani kuirudia, mwislamu simfutu Kila mtu tini zake, taratibu apitie. Mwisho iwe tathmini, matendo kijichunguza Dhububu tuwe tobani, ulokole kuukuza Si miujiza kubuni, wahubiri kujitembeza Muhimu sasa likizo, dhehebu zote zipewe! Malenga wa Vilimani (Kelvin K. M) Agosti thelathini, twenti twenti sigsi