
Uchomapo wajichoma Uendapo likizoni, kaite nafsi yako Nenda keti faraghani, pamoja kaa kitako Jimulike mja ndani, ukione kilichoko Ujipongeze galacha, heko shule kuichoma! Lipi mwana uwazile, kutawaliwa na choyo? Uchomapo yako shule, yaungua nafusiyo Moto uliomo mle, jivu utakuwa moyo Jipi bora upatile, kuteketeza wenzio? Hendi bure pulikiza, mchoma mastakimu Iwe mchana ni kiza, kulifanya la haramu Wenzio kuwaumiza, waandaa yako zamu Mja kulitenda jambo, mwenyewe ajitendea Moshi ule ulovuka, pako macho hautoki Vilio kutamauka, sikio haviondoki Moyoni mumefanyika, jukwaa havifutiki Dhamiri itakusuta, milele iwe gereza Moto huno wa mauti, hushtuki kukumbuka? Na msondo wa sauti, bweni likiporomoka Wendo kuwa mahututi, kwa moto ulioka Ukajiona ndo bingwa, kwa kutenda ushetani? Enenda mwana haramu, utubu zako dhunubu Viganjavyo vina sumu, na moyo una aibu Talipuka kama bomu, na mengi yakakusibu Kama toba hutofanya, uuswafi moyo wako Wajapo lilia haki, dhamiri itakubinya Ikuponde uwe baki, kwa kuchaze kukumenya Uwe meshika tariki, kichaa kupata mwanya Ndoto yako umechoma, na kesho kuboronganya KELVIN KOMBO MOTUKA (Malenga wa Vilimani) Aprili kumi na moja twenti twenti wani

