Bendera ya Kiswahili Kiswahili saba saba, kila mwaka ndiyo yake, Nafasi yake si haba, tambua mchango wake, Kina mengi matilaba, inajuzu kitumike, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Ndicho titi lake mama, Kiswahili kwa utamu, Mbele chazidi kuvuma, katika nyanja muhimu, Kiswahili kina noma, nembo Afrika humu, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Wasitoke kule kwao, wakibebee mgwisho, Na wenyeji tuwe ndio, twakithamini wa mwisho, Ndio usaliti huo, kwa makuzi ndilo tisho, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Leo kote ulimwengu, taa yake inawaka, Nawe vivyo msenangu, huna budi wajibika, Washa wondoe ukungu, lugha yetu kutumika, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Anuwai tunga kazi, nudhuma kila aina, Halisi na bunilizi, kwa mbinu kila namna, Tuchangie maenezi, lugha yetu kila kona, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Chipukizi na wasomi, ungana wanazuoni, Itengenezeni lami, tuingie safarini, Sote sio akisami, lugha yende kileleni, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Madhali ni sabasaba, beti saba sitazidi, Sizidi iwe hotuba, kukoma imenibidi, Chetu naweka akiba, hiyo ndo yangu ahadi, Bendera ya Kiswahili, Sabasaba ipepee! Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka) Julai 7, 2023