Song Cover Image

Vilio sampuli

Wanotaka hujawapa, wasotaka ukawapa Wakaona ni mfupa, kuguguna wanakwepa Wengi wao wanatupa, baraka ulizowapa Vino vilio sampuli, yote hayo majaliwa (Yatulizao majambo, mengi yatupigayo kumbo Kila siku ndio wimbo, kuwa mja ndiyo nembo) 2 Wapo uliwaonjesha, kisha kawashajiisha Nafsi kuwaridhisha, ikawa kuwauhisha Chozi wakapukutisha, kataraji kunyonyesha Wakaishia kulia, baraka kuipoteza Wengine wana banguzi, wanausuta uzazi Watekewa na malezi, kwa watoto wapuuzi Wanakwenda kaskazi, kukosea maamuzi Wana vilio sampuli, watoto wanawaliza Walopewa wa kiume, watamani wawakome Kitaka wajisukume, wende shuleni wasome Hawendi shamba walime, wajiona wanaume Ndivo vilio sampuli, vinavyosikika kote Wa kike waliovyaa,walalama ni balaa Wakabiliwa na baa, uvyazi wanajutia Wataka kuwa huria, ulimwengu kuchezea Moja wasilolijua, misiba wajisombea Walioko kwenye ndoa, wataka kujiondoa Wadai kujikomboa, madhila kuyakimbia Wanatoka wakilia, lengo lao kutulia Wanatoka kwenye moto, kutua kwenye tanuri Tele wapo wanaomba, wawe katika uchumba Wafike kwenye unyumba, wawe jiko au nyumba Upweke unowakumba, wautupe kama gamba Wauasi ukapera, familia waijenge Malenga wa Vilimani Kelvin Kombo Motuka (Septemba, 2022)