
Nimetakalamu, kwa kalamu yenye gundi Nimetakalamu, lienee kama bendi Nimetakalamu, lituwe yote makundi Nimetakalamu, kitegemea ushindi. Shikilo mwendo, ombi langu nitegee Shikilo mwendo, langu neno sipuzie Shikilo mwendo, roho yako lifungue Shikilo mwendo, kama kutu liondoe. Pamwe tangu, tumekuwa ni wandani Pamwe tangu, mekula moja sahani Pamwe tangu, kicheko cha hadharani Pamwe tangu, sikujua mimi kuni. Moyo kanama chupa, janga limedhihirisha Moyo kanama chupa, kichekoni wageresha Moyo kanama chupa, ndilo nimejifundisha Moyo kanama chupa, janga limenijulisha. Asekufaa kwa dhiki, yumkini mzandiki Asekufaa kwa dhiki, karamu sikupe uki Asekufaa kwa dhiki, cheko lake sisadiki Asekufaa kwa dhiki, si rafiki mutlaki. Nipo pweke nimejua, kovu peke nauguza Nipo pweke natambua, sinaye wa kunipoza Nipo pweke nishajua, tumbo linaponiliza Nipo pweke metambua, natapatapa kwa kiza. Kosa kubwa hapa chini, jua kuamini waja Kosa kubwa kibaini, hungoji yao faraja Kosa kubwa mwafulani, kupumbazwa na makoja Kosa kubwa walakini, ni kuichoma daraja. Bahari kuwa shwari, wanamaji si stadi Bahari kuwa shwari, hiyo mbovu itikadi Bahari kuwa shwari, mja huweki juhudi Bahari kuwa shwari, ni ajizi bila chudi. Akuangushaye mja, hukufunda kupigana Akuangushaye mja, hukomaza kikubana Akuangushaye mja, mshukuru si kuguna Akuangushaye mja, hukufunda kuchuana. Mja likuepukalo, jua nawe lina heri Mja likuepukalo, ujue ni makuduri Mja likuepukalo, witikiye ni kadari Mja likuepukalo, ni ridhaa ya Qahari. Kelvin Kombo Motuka (Malenga wa Vilimani) Nyamataro. Juni thatini, twenti twenti

