Niwambiaje wenzangu, wa mbali na wa karibu? Mwendo nahisi uchungu, kuwa sina la kujibu Waliotujua tangu, mamwinyi katuhesabu Niwaambe nini leo, kwamba vyote katoweka? Niwambiaje watokao, kuno kunako mavumbi Waja toka maeneo, ya minazi na makumbi Matunda wafuatao, niambe tunazo kumbi? Hatuna zaraa ati, ni majengo yalokitwa? Niwambiaje semeni, kwamba kuna maghorofa Na wengi ni masikini, walolimbuka ulofa? Maisha kwa kuwa duni, watembea japo kafa Chakula hawakimudu, kilimo ni marehemu? Niwambiaje viazi, na parachichi hakuna? Tunaagiza ndizi, hatupandi tukavuna Niwambie siku hizi, mchanga sio hazina Twakumbatia usasa, unotukuza viwanda? Niwambiaje yakini, soko halina perege? Vijaile gulioni, feki hata maharage Lipo tatizo majini, latowesha hata ndege Tuzile plastiki, badili ya kula nswi? Niwambiaje kizuru, mikononi wana chondo? Niwapeni washukuru, nami nione uhondo Nafusini niwe huru, kufurahia matendo Ama nikashifu Afrika, kwa kuandama usasa? Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka) Oktoba fiftini, twenti twenti tuu