
Shime Rais Uhuru! Twafika kwenye kilinge, tufungue sifungue, Uchumi wetu tujenge, taifa tulifufue? Wayafungue magenge, au wachwe waumie? Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Lifunga nchi kwa tone, idadi sasa yangalie Yazidi tamba senene, abadan sipungue Tweka chudi tuibane, korona katu situe Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Hofu imetamalaki, wengi raya situlie Na kihoro halaiki, chawafanya waugue Wanaikosa riziki, vipi ati wasilie? Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Mizozo ya kinyumbani, gani kisa sipungue, Kama sio hali duni, madeni siyaambae? Wamekuwa afkani, lino kufanya waue Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe Wanafuu na himila, jasisi mtuambie Hamira wengi wazila, matumbo mwisho yajae Wengi zawatia ila, ni muhali warejee Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe Mtyani wa kitaifa, na mbinguni niambie Nitolee taarifa, u'siano niujue Si kupima maarifa, duniani yakufae? Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Tumia yako hekima, huria tuachilie Raisi bora kupima, kwa busura uamue Twataka nasi kuchuma, kwa njaa siangamie Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Kiwa hapa daima, kuishi nayo tujue Tujenge kinga kukwima, korona itwepushie Kufungiwa ni gharama, inotuhasiri sie Shime Rais Uhuru, hima kafyu iondowe. Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka) 2020

