Lanifaa jina mbwa Nudhumu hino ni dua, ninaomba maghufira Pabaya natumbukia, Mkawini kukukera Nomba kunighofiria, si mwepesi wa hasira Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Mimi kweli mubwa mfu, hakika sina thamani Mhusika wa machafu, hadharani faraghani Kiumbe miye dhaifu, yanizonga yenye shani Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Wakitajwa wadhinibu, namba moja mimi ndiye Sherati ndiyo dhunubu, kunichochea niliye Yaniachia aibu, kunifanya niumiye Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Ungekuwa wahesabu, kutoa mara hukumu Ningekuwa kwa adhabu, duniani sipo humu Dhunubu zinanisibu, kwangu zikakuwa sumu Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Mungu umenirehemu, ukanipa ikibali Fadhili zako zadumu, dhunubu huzingatili Umenifanya muhimu, mja aliye halali Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Niepushie senene, unipe tena fursa Pupa mie niachane, vidimbwini kujitosa Moyo wangu ukapone, niepuke na mikasa Lanifaa jina mbwa, mtembea japo mfu Kelvin Kombo bin Motuka Malenga wa Vilimani. Desemba kumi na moja, twenti naintini