Korona Pele kwa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Akakosa kutulia, kwa muwasho kumchacha Matozi sishe kulia, kwa dhiki kutomuacha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Furisa hung'ang'ania, kutwa nzima hata kucha Dogo anoshikilia, hupokonywa kwa makucha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Fakiri lichopokea, humpoka anemucha Kifaidi meridhia, ao hao wenye kucha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa ’sokucha Hana la kufurahia, hata akipata vocha Wenye kucha hubambua, popote ajapoficha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Mashaka wampangia, utegemezi kwa tocha Halafu kusaidia, baadaye ndiyo picha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Ndiye kitovu cha njaa, sepata hata mchicha Mayowe anelalia, hana walau fanicha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Lebu wanojaribia, maponyo yote kwa necha Hawajali k'angamia, wana nini cha kukicha? Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Yamekuwa badalia, mebadilika kalicha Yote walitwamulia, macho leo wafikicha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Zimwi linawafagia, umayamaya ja kicha Nafuu tatupatia, kuvunjika kwa pakacha Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Ada tuliyozowea, pele kupawa 'sokucha Mpaka kuwasujudia, kuwaola magalacha Kwao tunakimbilia, ati uraiapacha! Pele safari hini, alopewa mwenye kucha Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka) 2020