WAMETOWEKA............ na Kelvin Motuka Twawatafuta walezi, kutoka yote mikoa Walezi walomaizi, kwamba malezi kikoa Wakawakosoa wazi, watoto pasi kujua Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Yale mawi yasoigwa, na kizazi yanafanywa Na vyakula hailigwa, vileo viwi wavinywa Kama si vyema kupigwa, kwani basi kutokanywa Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Hawathamini wazee, mifereji ya hekima Ni maneno wapapie, wakakosa usalama Wazazi wayajutie, mwisho ikija nakama Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Wakuavyo ni malezi, tariki waliyotiwa Si ajali si ulozi, vibaya kuangaliwa Kulea basi ndo kazi, wasotaka walipewa Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Walimu wajikunyata, la aula silabasi Wembe wao kijikata, ni wao na zao nafsi Wajisakie vitata, wafungie karatasi Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Wazazi toka kortini, nyumba zenu mrudie Keti nao sebuleni, wosia mwapatie Kutembea duniani, maadili wavalie Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Kwaheri mamu na dadi, lakabu za kudekeza Zinafifisha juhudi, kisha damu wakalaza Baadaye wakaidi, kwa kukosa kuwekeza Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Wazazi jitokezeni, muwe walezi hakika Watoto muwajengeni, nasaha kila dakika Wawe wana wa thamani, wasije kuhangaika Wametoweka walezi, kizazi kwenye mataa Malenga wa Vilimani