
Ndugu wa titi moja! Nani kawafunza wana, mloamwa ziwa moja? Kwa maelezo ya kina, mkaona ipo haja Mwache tangu kuonana, biashara tafrija Wakisii wa Nyamira, na Kisii kupigana? Kawafundisheni nani, funzo mkalielewa? Kwa mtindo wake gani, kisha mkalewalewa Kusahau mwafulani, nduguyo wa moja ziwa Akawa mwana haramu, asostahili urithi? Tini alowapa zipi, akilini kunakili? Mliandikia wapi, kiasi cha kutojali Na kuwaona makapi, ndugu zenu wa halali Majiwe kuwarushia, kama umbwa wa jirani? Huyo wenu mhadhiri, hakuwapani fasili? Ifanye mtafakari, kutunza ndugu asili Moja jambo kawaghuri, ndugu hasimu wa mbali Na anachostahili, ni mbali kufukuziwa? Basi wosia pulika, ndugu anayemfuma Huyo afahamu fika, la'na haitamkoma Kidosho wetu Keroka, kwa ujinga hatazama Anofaidi Keroka, wana wa mama mmoja! Malenga wa Vilimani (Kelvin Kombo Motuka) Machi nne, twenti twenti foomediu

